Na, Ernest Magashi
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Mhandisi Paskasi Muragili, ametoa siku 30 kwa vikundi vilivyonufaika na mikopo isiyo na riba kurejesha fedha hizo kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Mhandisi Muragili ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe alipokuwa akitoa maelekezo ya Serikali.
Alisema baadhi ya vikundi vimekuwa vikishindwa kurejesha mikopo waliyopewa, jambo linalokwamisha vikundi vingine kupata fursa ya kunufaika na mikopo hiyo.
“Baada ya siku 30 kuisha, vikundi vitakavyoshindwa kurejesha mikopo vitaanza kusakwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alisema Mhandisi Muragili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwaomba madiwani kwenda kuhamasisha vikundi katika maeneo yao kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili fedha hizo ziweze kuwafikia wananchi wengine wenye mahitaji ya mitaji ya kiuchumi.
Kagoma alisema vikundi vitakavyoshindwa kulipa kwa makusudi visiteteewe pale vitakapochukuliwa hatua za kisheria.
“Tusiviingilie vikundi vitakapoanza kukamatwa kwa kushindwa kurejesha mikopo. Fedha hizi zinapaswa kuwasaidia wananchi wengi zaidi kujikwamua kiuchumi,” alisema Kagoma.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alisema anatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa madiwani katika mikutano ya hadhara anayotarajia kuifanya kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mfikwa alisema madiwani watashirikishwa kikamilifu katika mikutano hiyo pamoja na kuendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kurejesha mikopo kwa wakati ili mfuko huo uweze kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.

Comments
Post a Comment