Na, Ernest Magashi
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Mhadisi Paskasi Muragili, amewaagiza watendaji wa kata zote 17 za Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kusimamia kwa karibu upatikanaji wa chakula katika shule za msingi na sekondari, hatua inayolenga kuboresha lishe, afya pamoja na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya wilaya kwa kipindi cha robo ya tatu (Januari hadi Machi) mwaka wa fedha 2025/2026, Mhadisi Muragili alisema lishe bora ni msingi muhimu wa ukuaji wa kiakili na kimwili kwa mwanafunzi, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha wanafunzi wanapata angalau mlo mmoja kamili wakiwa shuleni.
“Mwanafunzi hawezi kuwa makini darasani akiwa na njaa. Ni lazima tuhakikishe upatikanaji wa chakula shuleni unaimarishwa ili kujenga mazingira bora ya kujifunza na kuongeza ufaulu,” alisema Mhadisi Muragili.
Aidha, aliwataka watendaji wa kata pamoja na wadau wa elimu kuhakikisha utekelezaji wa afua za lishe mashuleni unazingatia mlo kamili wenye makundi yote muhimu ya chakula ikiwemo wanga, protini, vitamini na madini, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya ukuaji na kuimarisha kinga za mwili kwa wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amekitaka Kitengo cha Ukimwi Wilaya kuongeza juhudi katika utoaji wa huduma za upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU), pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa wanaotumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV).
Amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi na endelevu ya dawa hizo, akieleza kuwa uzingatiaji mzuri wa tiba husaidia kupunguza wingi wa virusi mwilini, kuboresha afya ya wagonjwa na kuzuia maambukizi mapya katika jamii.
Pia kikao hicho kiliweka mikakati ya kuunganisha juhudi za lishe bora, elimu na huduma za afya kama nguzo muhimu za kuboresha ustawi wa jamii na kuharakisha maendeleo endelevu kwa wananchi wa Wilaya ya Bukombe.

Comments
Post a Comment