CCM BUKOMBE YAMPONGEZA DKT. BITEKO KWA KUWAFIKIA WANACHAMA NA KUTOA SHUKRANI KWA UCHAGUZI WA RAIS SAMIA


Na, Ernest Magashi

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Matondo Lutonja, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kuwafikia wanachama na kutoa shukrani kufuatia ushindi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.Lutonja alitoa pongezi hizo wakati akimkaribisha Dkt. Biteko kuzungumza na wanachama wa CCM katika ziara yake iliyofanyika Kata ya Ng’anzo.Alisema Mbunge huyo amekuwa na utaratibu wa mara kwa mara wa kuwasalimia wapiga kura wake kupitia mikutano ya hadhara na makundi mbalimbali, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi. 

Hata hivyo, alibainisha kuwa ziara ya safari hii imekuwa ya kipekee kutokana na lengo la kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM, jambo linalozidi kumjengea imani na kukubalika kwa wananchi.

“Tunamkumbuka Dkt. Biteko alikuwa hapa mwezi uliopita, na sasa ndani ya muda mfupi amerudi tena kutusikiliza. Hii inaonesha jinsi anavyojali wananchi wake. Hakika anatufaa na tunapaswa kumuombea ili afanikishe zaidi maendeleo ya jimbo letu,” alisema Lutonja.Aidha, Lutonja alisema CCM Wilaya ya Bukombe inaridhishwa na utendaji wa mbunge huyo, akieleza kuwa ameendelea kuwaunganisha wananchi kupitia shughuli za kijamii huku akihimiza umoja, upendo na mshikamano.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea vizuri, huku miradi mingi iliyokuwa imeahidiwa ikianza kutekelezwa, akitolea mfano ujenzi wa zahanati katika maeneo ya Ituga na Butinzya, ambako tayari mbunge amechangia fedha.Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe, Leonard Mwakalukwa, alisema Tanzania ina mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini CCM ndicho chama chenye mvuto na uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.

“CCM ndicho chama kilichobeba matumaini ya Watanzania. Kina dira ya maendeleo na ndicho kinachoongoza serikali, hivyo ni wajibu wa viongozi wake kuendelea kukisemea na kukijenga,” alisema Mwakalukwa.Akizungumza na wananchi wa Ng’anzo, Dkt. Biteko alisisitiza kuwa ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu zitatekelezwa. Pia aliahidi kuchangia bati zote za kuezekea Zahanati ya Kazibizyo, ambayo wananchi tayari wamekamilisha ujenzi wa boma“Kazi ya mbunge ni kuunga mkono juhudi za wananchi. Nawaahidi kuleta bati zote za kuezekea zahanati mlioianzisha kwa nguvu zenu. Na kwa kuwa kata hii ina umoja, nawaomba muendelee kudumisha mshikamano huo hata baada ya uchaguzi wa ndani ya chama mwakani,” alisema Dkt. Biteko.Naye Diwani wa Kata ya Ng’anzo, Mashaka Shing’wenda, alimshukuru Dkt. Biteko kwa mchango wake katika maendeleo ya kata hiyo, ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari ya kata, zahanati ya Mtinga (ambapo alitoa bati zote), pamoja na kusaidia ujenzi wa shule katika maeneo ya Kazibizyo, Mtakuja na Mwamadilana A.

Alisema juhudi hizo zimekuwa chachu ya maendeleo na zimeendelea kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.

Comments