ZAHANATI YA NAMPALAHALA KUPANDISHWA HADHI KUWA KITUO CHA AFYA


Na, Ernest Magashi

Zahanati ya Kijiji cha Nampalahala, Kata ya Busonzo, Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, inatarajiwa kupandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya kufuatia Serikali kutoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu.Akizungumza wakati wa usimamizi wa ujenzi huo, Diwani wa Kata ya Busonzo, John Lugunya, alisema kuwa tayari kazi ya ujenzi imeanza, ikihusisha majengo muhimu yatakayowezesha zahanati hiyo kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya.Alieleza kuwa fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya nchini.Lugunya aliongeza kuwa zahanati hiyo ilianzishwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, pamoja na wadau wa maendeleo wakiwemo STAMIGOLD ambao walisaidia kukamilisha ujenzi wa awali wa zahanati hiyo.Kwa sasa, ujenzi unaoendelea unahusisha majengo ya Maabara na OPD, ambayo ni muhimu katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.Aidha, Lugunya alibainisha kuwa Mbunge Dkt. Doto Biteko alichangia vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 7, vikiwemo tofali, nondo na saruji, huku wananchi wakishiriki kikamilifu katika ujenzi huo.Kutokana na ukosefu wa kituo cha afya katika kata hiyo, wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu, hususan wanawake na watoto, kufuata huduma katika vituo vya jirani na Hospitali ya Runzewe.Akizungumzia maendeleo ya ujenzi huo, Mganga Mkuu Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Baraka Materu, alisema kuwa kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza changamoto ya umbali kwa wananchi.Kwa upande wake, Mbunge Dkt. Doto Biteko wakati ziara yake hivi karibuni kata ya Busonzo alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaendelea kwa vitendo.

Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na kuibua miradi ya maendeleo pamoja na kujitolea ili kuvutia uwekezaji zaidi wa Serikali katika eneo hilo.

Comments