Na, Ernest Magashi
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo na makampuni ya Equinor Tanzania AS na Shell Exploration and Production Tanzania Ltd kuhusu utekelezaji wa mradi wa gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) katika mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Kikao hicho kimefanyika leo Aprili 10, 2026, jijini Dar es Salaam, kikihusisha viongozi wakuu wa makampuni hayo, akiwemo Menno Bax, Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Shell Exploration and Production Tanzania Ltd, pamoja na Hilde Merete Nafstad, Makamu wa Rais na Meneja wa Nchi wa Utafutaji na Uzalishaji wa Kimataifa (EPI) wa Equinor Tanzania AS.
Mazungumzo hayo pia yaliwashirikisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, James Mataragio, pamoja na Kamishna wa Mafuta na Gesi kutoka Wizara hiyo, Goodluck Shirima.
Makampuni hayo yanajihusisha na shughuli za utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi asilia katika maeneo ya bahari kuu, pamoja na kushiriki katika maandalizi na utekelezaji wa mradi wa LNG unaotarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.

Comments
Post a Comment