Wataalamu kutoka idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamepatiwa mafunzo maalum ya uandaaji wa mpango mkakati wa miaka mitano, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mafunzo hayo yametolewa Aprili 14, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, yakiongozwa na mkufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Ngussa Kinamhila. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu katika matumizi ya mbinu za kisasa za kupanga, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi kwa ufanisi na weledi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mwezeshaji alisisitiza kuwa uandaaji wa mpango mkakati ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu. Alibainisha kuwa kupitia mafunzo hayo, wataalamu watawezeshwa kupanga bajeti, kusimamia utekelezaji wa miradi pamoja na kufanya ufuatiliaji wenye tija, ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi kwa manufaa ya wananchi wa Bukombe.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa maarifa wanayoyapata yatawasaidia kuandaa mpango mkakati unaozingatia vipaumbele vya maendeleo ya jamii na matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo.
Mafunzo hayo, yanayotolewa na wataalamu kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu, yakilenga kuimarisha maandalizi ya mpango mkakati wa Halmashauri kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2026 hadi 2031.

Comments
Post a Comment