Wananchi wa Kata ya Katente, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamejitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la kusafisha eneo litakalojengwa jengo la huduma za uzazi katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe. Ushiriki huo unaakisi mwamko mkubwa wa jamii katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya, hususan kwa mama na mtoto.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Marycelina Mbohoma, ametoa shukrani za dhati kwa Rais kwa kuidhinisha utoaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo muhimu. Amesema uwekezaji huo ni hatua madhubuti katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.
Aidha, Mbohoma amewataka wananchi kuendelea kuwa walinzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.“Mradi huu ni wetu sote. Ni wajibu wetu kuulinda, kuuthamini na kutoa taarifa mapema pale tutakapoona viashiria vya hujuma,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Ujenzi wa Wilaya, Haruni Fashe, amesema jengo hilo la kisasa litagharimu shilingi milioni 660 na linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi minne.
Amefafanua kuwa jengo hilo litakuwa na miundombinu muhimu ikiwemo wodi za wazazi, vyumba vya kujifungulia, chumba cha upasuaji, pamoja na huduma za watoto wachanga.
Mradi huu unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya wilayani Bukombe, kwa kuhakikisha akina mama wanapata huduma salama na bora wakati wa kujifungua, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyoweza kuzuilika.
Ushiriki wa wananchi katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu ni ishara ya umiliki wa kweli wa miradi ya maendeleo na msingi imara wa mafanikio endelevu ya sekta ya afya.
Mkazi wa Katente, Evodia Simon,alisema wamejitokeza kujitolea nguvu zao kama sehemu ya kuitikia wito wa maendeleo unaotolewa mara kwa mara na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, na viongozi wengine wa serikali katika mikutano ya hadhara.

Comments
Post a Comment