Wananchi wa Kijiji cha Busonzo, Kata ya Busonzo, Tarafa ya Siloka wilayani Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstafu, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake katika ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Busonzo, Victor Bwila, alimshukuru Dkt. Biteko kwa mchango wake mkubwa, akieleza kuwa ni kiongozi anayeonyesha kwa vitendo dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa CCM Kata ya Busonzo ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Matulanya Ngh’olombi, alisema Mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo na kuwafanya wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya kijamii, hususan ya afya.
Aliongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge pamoja na Diwani wa kata hiyo umewezesha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo.
“Chama Cha Mapinduzi kata ya Busonzo kinajivunia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na ushirikiano mzuri na viongozi wetu wa ngazi ya jimbo na kata, hali inayochochea maendeleo kwa wananchi,” alisema Ngh’olombi.
Aidha, alieleza kuwa kabla ya mwaka 2015, kata hiyo ilikuwa nyuma katika huduma za afya, lakini kwa sasa imepiga hatua kubwa kwa kuwa na shule, huduma za maji, vituo vya afya pamoja na ujenzi wa barabara unaoendelea.
Diwani wa Kata ya Busonzo, John Lugunya, alisema ujenzi wa zahanati hiyo ulianzishwa kwa nguvu za wananchi, huku ukichochewa kwa kiasi kikubwa na Mbunge Dkt. Biteko kupitia uhamasishaji na mchango wake wa fedha pamoja na vifaa vya ujenzi, ikiwemo mabati.
Alibainisha kuwa hadi kukamilika kwake, mradi huo unatarajiwa kugharimu takribani shilingi milioni 60, na kuongeza kuwa mchango wa Mbunge katika maendeleo ya kata hiyo umeonekana katika sekta mbalimbali.
“Awali kabla ya mwaka 2015, kata hii haikuwa na huduma za afya, lakini sasa kila kijiji kina zahanati, na ujenzi wa kituo cha afya unaendelea,” alisema Lugunya.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Busonzo, Godfrey Leonard, akifafanua hatua ya utekelezaji wa mradi huo, alisema pamoja na mchango wa Mbunge, wadau wa maendeleo wakiwemo Kampuni ya BXC wamechangia kukamilisha ujenzi huo. Pia fedha kutoka Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimewezesha ujenzi wa kichomea taka pamoja na vyoo.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa zahanati hiyo kutapunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika vijiji jirani, hasa kwa wanawake na watoto.

Comments
Post a Comment