Serikali imewataka Wakaguzi Wakuu wa Migodi pamoja na Mameneja wa Migodi nchini kuwa mabalozi wa utekelezaji wa sheria na kanuni za madini, huku wakihimizwa kuonesha uzalendo katika kusimamia biashara halali ya madini ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Wito huo umetolewa Aprili 24, 2026 wilayani Kahama, mkoani Shinyanga na Mtaalam kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini, Tume ya Madini, Mhandisi Erasmina Massawe, wakati akifungua mafunzo kwa Mameneja na Wakaguzi Wakuu wa Migodi ya uchimbaji mdogo.
Mafunzo hayo yamewakutanisha washiriki kutoka maeneo ya kimadini ya Kahama, Mbogwe na Shinyanga.Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uelewa wa kitaalam, kuboresha usimamizi wa migodi, kuongeza uzingatiaji wa sheria na kanuni za madini pamoja na kukuza uchimbaji salama na endelevu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mhandisi Massawe alisema mbali na kujengewa uwezo wa kitaalam, viongozi hao wanapaswa kuwa sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali inayolenga kuhakikisha biashara ya madini inafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia Sheria ya Madini na kanuni zake, hatua itakayosaidia kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo kwa kutekeleza mikakati mbalimbali, ikiwemo uboreshaji wa mfumo wa biashara ya madini, uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, uwepo wa Maafisa Migodi Wakazi katika maeneo ya uchimbaji pamoja na ujenzi wa ukuta wa Mirerani uliosaidia kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite.
Aidha, Serikali imeimarisha ulinzi na ufuatiliaji wa madini kwa kuweka wakaguzi katika maeneo muhimu kama viwanja vya ndege, bandari na mipakani, sambamba na kusimamia utoaji wa vibali vya usafirishaji wa madini na utekelezaji wa sheria za kodi, ikiwemo ondoleo la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye baadhi ya shughuli za madini.
Akizungumzia ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo, Mhandisi Massawe alisema maboresho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania yameongeza kwa kiasi kikubwa fursa kwa wazawa kushiriki katika usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali migodini.
“Kwa sasa zipo fursa nyingi katika sekta ya madini, ikiwemo huduma za chakula, ulinzi, vifaa vya kinga, huduma za kisheria, ujenzi na bima. Watanzania wanapaswa kuzitumia fursa hizi kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa nchi,” alisema.
Wakati huo huo, amehimiza wadau wa madini kutumia maabara ya kisasa ya Tume ya Madini iliyopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya upimaji wa madini na sampuli zake, ili kuhakikisha biashara ya madini inafanyika kwa uhakika na uaminifu.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usimamizi wa uchimbaji mdogo na kuhakikisha rasilimali za madini zinaleta manufaa mapana kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Comments
Post a Comment