Na, Ernest Magashi
Serikali imedhamiria kuhakikisha vitongoji vyote 64,359 vya Tanzania Bara vinafikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030, hatua inayolenga kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuboresha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi vijijini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, Aprili 22, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika Bunge la 13, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Kumi na Nne.
Alisema kuwa ili kufikia azma hiyo, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kupeleka umeme katika vitongoji 9,009 unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu ijayo.
Aidha, alifafanua kuwa miradi inayoendelea kwa sasa itawezesha vitongoji 50,453, sawa na asilimia 78.4 ya vitongoji vyote vya Tanzania Bara, kufikiwa na umeme ifikapo mwaka 2028, hali itakayoongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini.
Waziri Deogratius Ndejembi alieleza kuwa hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa kuongeza uunganishaji wa wateja katika vitongoji (Universal Hamlet Electrification and Last Mile Connectivity) unaotekelezwa katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Dodoma. Mradi huo ni sehemu ya Mpango Mahsusi wa Nishati wa Taifa (National Energy Compact) ulioridhiwa katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika (Mission 300) uliofanyika Januari 2025.
Hatua nyingine ni utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 3,060 (sawa na vitongoji 15 kwa kila jimbo), ambao umefikia takribani asilimia 80 ya utekelezaji.
Pia, Serikali inaendelea kusambaza umeme katika mikoa ya Songwe, Kigoma na Lindi, pamoja na maeneo ya migodi midogo kama Chunya (Mbeya) na Kwa Msisi (Handeni Tanga), sambamba na kuimarisha nishati katika viwanda vya kilimo katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Rukwa.
Katika kuhakikisha maeneo yaliyo mbali na gridi ya taifa yanafikiwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kusambaza mifumo ya umeme wa jua (Solar Home Systems SHS) kwa kaya 20,000 katika visiwa vidogo 143 vilivyopo Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika. Hadi Machi 2026, jumla ya kaya 1,302 zilikuwa zimefungiwa mifumo hiyo.
Akizungumzia nishati safi ya kupikia, Waziri Ndejembi alisema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 2034) uliozinduliwa Mei 2024, unaolenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Alibainisha kuwa jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda, ambapo matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, hatua inayosaidia kulinda mazingira na afya za wananchi.
Kwa upande wake, Waziri huyo alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti unaochochea upatikanaji wa nishati safi na endelevu nchini, akisema juhudi hizo zimemfanya kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia barani Afrika na kimataifa.
Wabunge mbalimbali, wakichangia mjadala huo, walimpongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa mafanikio katika kusambaza umeme vijijini pamoja na kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Comments
Post a Comment