RUWASA BUKOMBE YABORESHA HUDUMA YA MAJI


Na, Ernest Magashi

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, umeanza rasmi utekelezaji wa mfumo wa kisasa wa utoaji huduma ya maji kwa kuzindua matumizi ya mita za maji za malipo kabla ya matumizi (prepaid meters).Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bukombe, Mhandisi James Benny, alisema kuwa mfumo huo utaleta uwazi na uwajibikaji kwa watumiaji wa huduma ya maji, huku ukiondoa malalamiko ya bili zisizo sahihi. Aidha, utaimarisha ukusanyaji wa mapato na kupunguza changamoto ya madeni ya wateja.“Kwa kutumia mita hizi za kisasa, mteja atalipia huduma kabla ya kutumia maji. Hii itasaidia kudhibiti matumizi holela na kuhakikisha kila mwananchi analipia kiwango halisi anachotumia,” alisema Mhandisi Benny. Aliongeza kuwa mfumo huo unampa mteja uhuru wa kupanga matumizi yake kulingana na uwezo wake wa kifedha.Alifafanua kuwa katika hatua za awali, RUWASA imeanza kufunga mita hizo katika taasisi za umma ili kuhakikisha mfumo unaanza kutumika kwa ufanisi na kuwa mfano kwa jamii.“Kuanzia leo, tumefanikiwa kufunga mita ya maji ya malipo kabla ya matumizi katika Zahanati ya Bukombe. Hii ni hatua ya mwanzo kabla ya kuendelea na taasisi nyingine za umma na hatimaye kuwafikia wananchi wote,” alieleza.

Mhandisi Benny alibainisha kuwa RUWASA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mita hizo, ikiwemo namna ya kununua na kujaza salio, ili kuhakikisha kila mtumiaji ananufaika kikamilifu na mfumo huo wa kisasa.Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bukombe, Dkt. Hassani Hamis, alipongeza hatua hiyo akisema imekuja kwa wakati muafaka, kwani itarahisisha malipo ya maji kulingana na matumizi halisi ya taasisi hiyo.

Uzinduzi wa mita hizo umefanyika kufuatia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza matumizi ya mita za malipo kabla ya matumizi kama njia ya kudhibiti changamoto ya bili za kubambikiziwa zinazotokana na vitendo vya baadhi ya watumishi wasio waadilifu.

Comments