Abubakari Msita- Bukombe, Geita | 1 Aprili 2026
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Bukombe amewataka vijana wilayani humo kuwa wazalendo na kutumia ipasavyo fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana ndani ya wilaya hiyo ili kujiletea maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla.
Akizungumza leo katika kata ya Bulangwa, wakati akiendelea na ziara yake ya kutembelea na kukagua uhai wa jumuiya hiyo, kiongozi huyo amesema vijana wana nafasi kubwa ya kuwa nguvu kazi ya taifa endapo wataamua kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo, ufugaji na ujasiriamali.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa vijana kuendelea kushikamana na kushiriki kikamilifu katika shughuli za jumuiya pamoja na maendeleo ya Chama, huku akiwataka viongozi wa ngazi za chini kuhakikisha wanadumisha uhai wa jumuiya na kusimamia maslahi ya vijana.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha jumuiya, kusikiliza changamoto za vijana, pamoja na kuweka mikakati ya kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi ndani ya Wilaya ya Bukombe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa kata hiyo ya Bulangwa Ndg Alex Marcel ameahidi kuendelea kuwaunganisha vijana wa eneo hilo, kuhamasisha mshikamano, pamoja na kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na jumuiya hiyo ili kuimarisha zaidi uhai na nguvu ya UVCCM katika kata hiyo.
Amesema kupitia umoja huo, vijana wengi zaidi wataweza kupata jukwaa la kujadili changamoto zao, kubadilishana mawazo ya maendeleo na kushiriki kikamilifu katika fursa za kiuchumi na kijamii zinazopatikana katika Wilaya ya Bukombe.




Comments
Post a Comment