MRADI WA WASH KULETA MAPINDUZI YA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Wilaya ya Bukombe wanatarajia kupata nafuu ya changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia utekelezaji wa mradi wa Maji, Afya na Usafi wa Mazingira (WASH) ulioanza Machi 2026 na unatarajiwa kukamilika Februari 2027.Mradi huo unatekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Community Based Health Care Council (CBHCC) lenye makao makuu jijini Arusha, kwa kushirikiana na Wizara ya Maji pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.Akizungumza wakati wa hafla ya utambulisho wa mradi huo, Meneja wa CBHCC, Said Said, alisema lengo kuu la mradi ni kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama, kuimarisha afya ya jamii, na kuinua kiwango cha usafi wa mazingira ili kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama.Alifafanua kuwa katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji, mradi unahusisha vijiji kumi ambavyo ni Bulama B, Nampangwe B, Ikalanga Senta, Kakoyoyo (Mgombani), Kakoyoyo (Elimu), Nalusinguti, Ilalwe (Migamba), Miyenze (Msindikwa), Bufanka Senta pamoja na Bugando (Bukamba).Said alibainisha kuwa mradi huo utachangia kuongeza upatikanaji wa maji safi vijijini, kuboresha afya za wananchi, na kuimarisha usafi wa mazingira. Aidha, utaongeza ufanisi wa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO) kupitia mafunzo na ufuatiliaji wa karibu.Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa CBHCC, Pendo Sakafu, alisema ubora wa maji utakuwa ukifuatiliwa kwa karibu kupitia vipimo vya mara kwa mara vitakavyofanyika katika maabara zilizoidhinishwa, ili kuhakikisha maji yanayotolewa yanakidhi viwango vya kitaifa.Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bukombe, Mhandisi James Benny, alisema mradi huo ni suluhisho muhimu kwa changamoto ya maji katika wilaya hiyo.“Tunaushukuru mradi huu kwa kuja katika Wilaya yetu. Tunaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza, au hata kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama. Sisi kama RUWASA tupo tayari kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wake,” alisema.

 

Comments