Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM) ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita, imewataka wawekezaji wa sekta ya madini kuhakikisha wanazingatia utunzaji wa mazingira sambamba na kulipa tozo na ushuru kwa wakati, ili kuongeza mapato ya ndani na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alipokuwa akiongoza kamati hiyo katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya wawekezaji wa madini ya dhahabu katika Kata ya Igulwa, Tarafa ya Ushirombo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kagoma alisisitiza kuwa ulipaji wa tozo kwa wakati ni wajibu wa kila mwekezaji na mtoa huduma katika sekta ya madini.
“Mapato haya ndiyo msingi wa uendeshaji wa Halmashauri na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi,” alisema Kagoma.
Alieleza kuwa ziara hiyo imelenga kukagua na kutathmini vyanzo vya mapato vinavyotokana na shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu, pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuhakikisha shughuli hizo zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kimazingira.
Maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na mitambo ya uchenjuaji, mialo na makarasha katika maeneo ya Kasaka (Kata ya Igulwa Kelezia), Bulama na Musasa.
Kamati ilipata fursa ya kujionea mwenendo wa shughuli hizo, ikiwemo matumizi ya kemikali na mifumo ya usimamizi wa mabaki yatokanayo na uchakataji.
Katika hatua ya kulinda mazingira, kamati imeelekeza wamiliki wa mitambo ya uchenjuaji kuhakikisha wanaweka miundombinu madhubuti ya kudhibiti maji taka yenye kemikali, ikiwemo ujenzi wa mabwawa na mifereji maalum kuzunguka maeneo ya miradi.
Hatua hiyo inalenga kuzuia kusambaa kwa kemikali hatarishi kama zebaki na sianidi, ambazo zinaweza kuathiri afya za wananchi na mfumo wa ikolojia, hasa wakati wa msimu wa mvua.
Aidha, kamati imesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uzio katika maeneo ya shughuli za madini ili kuzuia mwingiliano kati ya maeneo ya kazi na makazi ya wananchi. Imeonya kuwa matumizi yasiyo salama ya kemikali yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu na viumbe hai.
Ziara hiyo imebainisha umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini katika ngazi ya Halmashauri kwa kuzingatia misingi ya uchimbaji endelevu, ili kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi bila kuhatarisha mazingira na afya za wananchi.
Kamati imeeleza dhamira yake ya kuendelea kusimamia sekta ya madini kwa weledi, uwajibikaji na ufanisi, huku ikihimiza ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Comments
Post a Comment