Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Dkt. Deograsia Mkapa (MD, MSc Epidemiolojia), ametunukiwa tuzo ya Mwanamke Kinara Kanda ya Ziwa 2026 kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya na maendeleo ya jamii.
Dkt. Mkapa, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania, ametambuliwa miongoni mwa wanawake waliotoa mchango wa kipekee katika sekta mbalimbali. Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla iliyofanyika jijini Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, aliwapongeza wanawake wote waliotunukiwa tuzo kwa juhudi zao kubwa katika kuleta maendeleo chanya ndani ya jamii.
Dkt. Mkapa alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya sekta ya afya, akitambuliwa kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za afya pamoja na kupambana na magonjwa mbalimbali katika jamii.
Kwa mujibu wa wasifu wake wa kitaaluma, Dkt. Mkapa ni mtaalamu wa Epidemiolojia mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika utoaji wa huduma za afya nchini Tanzania, akihudumu katika ngazi mbalimbali za vituo vya afya.
Aidha, ana uzoefu mkubwa katika udhibiti na ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko pamoja na yale yanayozuilika kwa chanjo. Hapo awali, aliwahi kufanya kazi kama mtaalamu mshauri chini ya mradi wa Task Force for Global Health, kwa kushirikiana na U.S. Centers for Disease Control and Prevention (CDC), ambapo alitoa mchango muhimu katika kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 katika mikoa ya Geita na Kagera.
Kwa sasa, akiwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Mkapa anasimamia utoaji wa huduma za afya, ikiwa ni pamoja na matibabu, uchunguzi na udhibiti wa magonjwa, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, zenye usawa na gharama nafuu.
Pia amejitokeza kuwa kinara katika kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, hususan saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake, kupitia utoaji wa elimu, chanjo na uchunguzi wa mapema.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Mkapa aliwashukuru wananchi na watumishi wenzake kwa kumuunga mkono na kumpigia kura.
“Nawashukuru sana wananchi na watumishi wenzangu kwa kunipigia kura na kunichagua kuwa Mwanamke Kinara Kanda ya Ziwa.Asanteni sana, na tuendelee kushirikiana siku zote,” amesema Dkt. Mkapa.
Tuzo ya Mwanamke Kinara Kanda ya Ziwa 2026 inalenga kutambua na kuthamini mchango wa wanawake wanaoleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu, uongozi na uchumi.

Comments
Post a Comment