DKT. BITEKO AWATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIKOPO

Na Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Doto Biteko, amewataka wananchi kuchangamkia fursa za mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri.Dkt. Biteko alitoa wito huo wakati wa ziara yake katika Kata ya Busonzo, alipokuwa akizungumza na wanachama na wananchi. Alisisitiza umuhimu wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuunda vikundi na kuvisajili kisheria ili waweze kunufaika na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya mikopo hiyo, kwa lengo la kukuza uchumi wao.Alieleza kuwa Halmashauri ya Bukombe inaongoza kwa utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa makundi hayo, na hivyo kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kubadili maisha yao.“Nawaomba wanachama kuendelea kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa za mikopo pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inaendelea kuleta fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali, shule na barabara ili wananchi wanufaike,” alisema Dkt. Biteko.Aidha, aliwataka wananchi kuchukua mikopo kwa uangalifu kwa kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuirejesha, ili kuepuka changamoto za kudaiwa baadaye.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema halmashauri imeendelea kutoa mikopo na hivi karibuni imetoa said ya shilingi milioni 196 kwa vikundi 26.Aliongeza kuwa kwa sasa kuna tangazo la utoaji wa zaidi ya shilingi milioni 256, na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na mikopo hiyo isiyo na riba kwa ajili ya kukuza uchumi wa familia zao.Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Narusungute, Kasema Lukaga, alimpongeza mbunge huyo kwa kuhamasisha maendeleo na kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu.Mkazi wa kijiji cha Nyakayenze, Lusia Kadoke, pia alimpongeza Dkt. Biteko kwa kufika kijijini hapo, kusikiliza wananchi na kuonesha kujali maendeleo yao.

Comments