DKT. BITEKO AWAPONGEZA WALIMU KWA KUINUA KIWANGO CHA ELIMU BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Doto Biteko, amewapongeza walimu wa shule za msingi na sekondari kwa juhudi zao za kufundisha vizuri wanafunzi, hatua iliyochangia kuinua kiwango cha ufaulu na kuifanya wilaya hiyo kufanya vizuri kitaaluma mkoani Geita.Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo baada ya Diwani wa Kata ya Runzewe Mashariki, Mery Nchiba, kueleza kuwa Shule ya Sekondari Ikunzi imepata matokeo mazuri katika mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2025. Kauli hiyo aliitoa wakati wa mkutano wa wanachama na wananchi uliofanyika katika ziara ya mbunge huyo ya kuwashukuru.Akiwapongeza walimu, Dkt. Biteko pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini, ikiwemo Wilaya ya Bukombe, hususan katika sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.Alisema uwekezaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuimarisha sekta ya elimu kwa ujumla. Aidha, aliwataka walimu na wanafunzi kuendelea kuongeza bidii ili kudumisha na kuboresha zaidi matokeo hayo mazuri.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Runzewe Mashariki, Mery Nchiba maarufu kama “Shangazi”, alibainisha kuwa Shule ya Sekondari Ikunzi imeonyesha mafanikio makubwa katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2025, jambo linaloonesha jitihada za walimu na wanafunzi.Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema serikali tayari imetoa shilingi bilioni 18 kwa halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.


Comments