Na Ernest Magashi
Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Bukombe na mkoani Geita kwa kazi kubwa waliyoifanya kufuatia tukio la kuzagaa kwa taarifa za kudaiwa watu kufukiwa katika mgodi wa Msasa Gold Mine.
Taarifa hizo zilizosambaa zilidai kuwepo kwa vifo katika mgodi huo, jambo lililozua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi, lakini baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na vyombo husika, imebainika kuwa hakukuwa na watu waliofariki dunia.
Dkt. Biteko amewaomba wananchi wa Bukombe kuendelea kuwa watulivu na kuviamini vyombo vya dola, akieleza kuwa tangu kutokea kwa tukio hilo, viongozi mbalimbali wa serikali, Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na wananchi na wachimbaji katika kuhakikisha ukweli unapatikana.
“Nawapongeza sana vyombo vya dola kwa ushirikiano mkubwa mliouonyesha kwa kufanya kazi usiku na mchana, mkijituma kufukua na kuchunguza eneo lililokuwa linadaiwa kufukiwa watu. Hatua hii imeleta utulivu mkubwa kwa wananchi,” alisema Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewapongeza waandishi wa habari mkoani Geita kwa kuripoti taarifa kwa weledi, ukweli na kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Alisema waandishi hao walifika eneo la tukio, kujionea hali halisi, kuzungumza na wahusika pamoja na wananchi, hatua iliyosaidia kutoa taarifa sahihi kwa umma na kuondoa upotoshaji.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita, Kenneth Mwakisitu, alisema juhudi za utafutaji zilifanyika kwa umakini mkubwa lakini hakuna mwili wa binadamu uliopatikana katika eneo hilo.
Naye Mkuu wa Idara ya Ukaguzi katika mgodi wa Msasa Gold Mine, James Balele maarufu “Ng'wana Kamba”, alithibitisha kuwa hakuna tukio la watu kufukiwa lililotokea mgodini hapo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Safia Jongo, aliwataka wananchi kupuuza taarifa zisizo na uhakika na kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani ikiwa tukio hilo lilitokea Machi 29,2026 majira ya sasa 4:30 asubuhi.

Comments
Post a Comment