DKT. BITEKO AOMBA USHIRIKIANO, ATOA WITO WA KUHAMASISHA MAENDELEO


Na Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Doto Biteko, amewaomba wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa mafanikio hupatikana kwa umoja na ushirikiano.Akizungumza katika ziara yake Kata ya Namonge, Dkt. Biteko, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, alisema ni wajibu wa wanachama kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hususan katika kuboresha huduma za kijamii na miundombinu.Katika ziara hiyo, alimpongeza Diwani wa Kata ya Namonge, Mlalu Bundala, kwa juhudi zake za kusikiliza na kuwasilisha kero za wananchi, akisema zimekuwa zikifanyiwa kazi kwa ushirikiano wa viongozi wa serikali.Dkt. Biteko pia aliwashukuru wananchi wa Bukombe kwa kumuamini Rais Samia pamoja na yeye binafsi kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao bungeni, akiahidi kuendelea kuwatumikia kwa uaminifu.“Kila maendeleo yanayofanyika Bukombe yanatokana na fedha zinazoletwa na Rais Samia. Ni kiongozi mwema anayejali wananchi wake, na nina hakika maendeleo makubwa zaidi yanakuja,” alisema.Aliwaomba wananchi wa Namonge kupokea shukrani zake pamoja na za Rais Samia, huku akiahidi kuwa ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni zitatekelezwa.Aidha, aliwataka viongozi wa chama kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, akibainisha kuwa Kata ya Namonge ina vijiji vinne vinavyohitaji kuwa na zahanati ili kupunguza adha ya wananchi, hususan wanawake na watoto, kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya. Alitaja pia vipaumbele vingine kuwa ni barabara, elimu, afya na maji.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri imepokea shilingi bilioni 18 kutoka serikalini kwa ajili ya miradi ya elimu, afya, barabara na maji. Aliwataka wananchi kuendelea kuisemea serikali kutokana na juhudi kubwa inazofanya katika kuwaletea maendeleo.Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kazi kubwa ya kuhamasisha maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano wake na Rais Samia umeleta mafanikio yanayoonekana kwa wananchi.

 

Comments