DKT. BITEKO AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUCHOCHEA MAENDELEO YA WANANCHI


Na, Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Doto Biteko, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa anazoendelea kufanya katika kuwaletea maendeleo wananchi kupitia Serikali ya Awamu ya Sita.Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa ziara yake tarafa ya Siloka iliyolenga kuwashukuru wananchi kwa ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 2025.Aidha, aliwataka wananchi na wanachama wa CCM kutunza ardhi zao, akieleza kuwa Wilaya ya Bukombe ina fursa kubwa za kiuchumi zinazokuja kutokana na miradi mikubwa ya maendeleo. Alitaja ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) pamoja na maendeleo ya bandari kavu ya Isaka kuwa ni miongoni mwa jitihada za Rais Samia katika kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Bukombe na maeneo jirani.Alisema miundombinu hiyo itahudumia pia nchi jirani zikiwemo Rwanda, Burundi, (DRC)  Congo na Uganda, hivyo kuongeza fursa za biashara na uwekezaji.“Ninapenda kuwashukuru sana wananchi kwa kunichagua mimi kuwa mwakilishi wenu pamoja na kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan na madiwani wenu. Asanteni sana kwa imani yenu,” alisema Dkt. Biteko.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Runzewe Magharibi, Patrick Songoro, alitaja changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo, akisema kwa sasa dumu moja la maji linauzwa hadi shilingi 500 kutokana na ongezeko la watu kufuatia shughuli za mgodi wa Msasa.

“Tulikuwa hatuna kituo cha afya, lakini sasa kinaendelea kukamilika. Pia kuna mradi wa maji wa Msasa, na zahanati ya Namsega tayari imeanza kutoa huduma,” alisema Songoro huku akimpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi zake za maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema jumla ya vikundi 23 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu tayari vimenufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri hiyo, hatua inayochochea maendeleo ya kiuchumi kwa makundi mbalimbali ya jamii.

Comments