DKT. BITEKO AHIMIZA USHIRIKIANO KUCHOCHEA MAENDELEO BUKOMBE

Na Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Doto Biteko, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi kushirikiana katika kuibua na kusimamia miradi ya maendeleo.Dkt. Biteko alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wanachama na wananchi wa Kata ya Runzewe Mashariki na Runzewe Magharibi, wakati wa ziara yake ya kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mbunge pamoja na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na madiwani wao.Alisema kuna umuhimu wa kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.“Mahali popote ambapo watu wameungana kwa pamoja, maendeleo huonekana kwa haraka,” alisema Dkt. Biteko.Aidha, alibainisha kuwa Wilaya ya Bukombe inaendelea kukua kiuchumi, na kuwataka wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri.Alisisitiza kuwa lengo lake ni kuona Bukombe inakuwa wilaya ya mfano kwa maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika miundombinu na ushirikiano wa wananchi.“Mmenipa heshima kubwa. Naomba ushirikiano wenu; pale ninapokosea nishauri ili nijirekebishe. Kwa kushirikiana na madiwani, tutahakikisha miradi yote ya maendeleo inakamilika, ikiwemo ujenzi wa shule na zahanati,” aliongeza.Dkt. Biteko pia aliwataka viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya shina hadi tawi kudumisha umoja, akisisitiza kuwa mshikamano ndio chachu ya maendeleo. Aidha, aliwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Ikunzi kwa kusimamia vizuri taaluma, hali iliyochangia kufanya vizuri kitaifa.

Dkt. Doto Biteko alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo Wilaya ya Bukombe ambayo imeendelea kunufaika na juhudi za serikali ya awamu ya sita.

 Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Runzewe Mashariki Mery Nchiba alisema wananchi wa kata hiyo wana hamu kubwa ya maendeleo na wanathamini ujio wa mbunge wao, huku akiwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wanapata elimu.Naye Diwani wa kata ya Runzewe Magharibi Patrick Songolo alimshukuru mbunge kwa ushirikiano wake mkubwa katika kutatua changamoto za wananchi, akitaja mafanikio yaliyopatikana ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya.

Alieleza kuwa hapo awali eneo hilo halikuwa na kituo cha afya, lakini sasa majengo yanaendelea kujengwa kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia.

Hata hivyo, alibainisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, akisema kisima kilichopo hakitoshelezi mahitaji ya wananchi.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema halmashauri imetenga shilingi milioni 256.8 kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aliongeza kuwa serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa shule, barabara na uboreshaji wa huduma za afya.

Comments