DIWANI AHIMIZA UTUNZAJI WA MAZINGIRA KWENYE VYANZO VYA MAJI


Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Kata ya Uyovu, Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamehimizwa kuendelea kutunza mazingira katika vyanzo vya maji ili kuepuka athari za ukame.Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Uyovu, Matayo Kagoma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la ofisi ya Chombo cha Watoa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (UYOVU-CBWSO).

Kagoma amesema kuwa ni muhimu kwa wananchi kuzingatia upandaji na utunzaji wa miti, hususan ile ya asili, kwani ina mchango mkubwa katika kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji.Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Bukombe, Mhandisi James Benny, amesema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kusisitiza kuwa miti iliyopandwa inapaswa kulindwa. Ameongeza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha CBWSO zote zinapata ofisi ili kuboresha utendaji kazi.Naye Kaimu Msimamizi wa UYOVU-CBWSO, Sakibu Sadick, ameshukuru kwa kupatikana kwa ofisi hiyo akisema itasaidia kupunguza msongamano wa wateja, kurahisisha shughuli za kila siku za usimamizi wa huduma za maji pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.Akizindua rasmi ofisi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, amesisitiza umuhimu wa kupanua mtandao wa maji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wa maeneo ya vijijini.Mhandisi Muragili amesema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa huduma za maji ngazi ya jamii. Ameongeza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopo, bado kuna haja ya kuongeza juhudi katika kupanua miundombinu ya maji ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.“Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya maji, lakini ushiriki wa wananchi na usimamizi madhubuti wa CBWSO ni nguzo muhimu ya mafanikio. Hakikisheni mnapanua mtandao wa maji ili kila mwananchi anufaike na huduma hii,” amesema Muragili.Aidha, amewapongeza UYOVU-CBWSO kwa kufanya vizuri na kushika nafasi ya tatu kati ya vyombo 931 vya utoaji huduma za maji nchini. Pia amewahimiza wananchi kufika ofisini hapo kuomba huduma ya maji ili waweze kusogezewa huduma hiyo karibu na makazi yao. 

Comments