DE-D AWAPIGA MSASA WATENDAJI WA KATA KUSIMAMIA MAREJESHO YA MIKOPO BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

Watendaji wa kata 17 wilayani Bukombe mkoani Geita wametakiwa kusimamia kwa karibu vikundi vinavyopokea mikopo kutoka Halmashauri, kwa lengo la kuhakikisha marejesho ya fedha hizo yanafanyika kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa kata pamoja na maafisa maendeleo ya jamii, akisisitiza umuhimu wa ufuatiliaji madhubuti wa marejesho ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.Mfikwa alisema mikopo hiyo inalenga kuinua uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii, hivyo ni wajibu wa watendaji kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa kwa wakati ili ziweze kuwafikia wanufaika wengine.

“Ni lazima kila mmoja awajibike kuhakikisha vikundi vinarejesha mikopo kwa wakati. Huu ni wajibu wa moja kwa moja na pia ni kipimo cha utendaji kazi wenu,” alisema Mfikwa.

Aidha, aliwataka watendaji kuweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji kwa kukusanya taarifa sahihi za marejesho na kuwasilisha mrejesho wa kila mwezi kuhusu hali ya mikopo hiyo.Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo aliwaelekeza watendaji wa kata kubainisha maeneo yote ya wazi ya serikali yaliyopo katika maeneo yao na kuhakikisha yanalindwa dhidi ya uvamizi au matumizi yasiyo halali.

Alisisitiza kuwa utambuzi na ulinzi wa maeneo hayo ni muhimu katika kulinda rasilimali za umma na kupanga maendeleo endelevu ya halmashauri.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bukombe, Melania Kwai, aliwataka maafisa maendeleo ya jamii kuongeza juhudi katika usimamizi wa vikundi kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji, ili kuhakikisha hakuna kikundi kinachochelewesha marejesho bila sababu za msingi.Kikao hicho kimefanyika wakati Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ikiendelea kuimarisha mikakati ya kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia usimamizi bora wa rasilimali za fedha.


Comments