Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Marycelina Mbehoma, amewakumbusha wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo endelevu.
Mbehoma ametoa wito huo wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo kwa vikundi 23 vyenye jumla ya wanachama 123 kutoka makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, vilivyonufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 196. Fedha hizo zinatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema kurejeshwa kwa mikopo hiyo kwa wakati kutaiwezesha halmashauri kuvikopesha vikundi vingine zaidi mikopo isiyo na riba, hatua itakayosaidia kukuza vipato vya familia na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Ally Mketo, alisema matarajio ya serikali ni kuona mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwa kuongeza kipato cha wanufaika na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alisema anajivunia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo inaendelea kuwagusa wananchi moja kwa moja kupitia uwezeshaji wa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Japhet John kutoka kikundi cha Peace Transport Group, aliishukuru serikali kwa kuwawezesha na kuahidi kuwa wataitumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa pamoja na kuirejesha kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, aliwapongeza wanufaika kwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na kuwataka kutumia fursa hiyo vizuri kwa maendeleo yao binafsi na ya jamii. Alisisitiza kuwa mikopo hiyo ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi na kusaidia familia kujikwamua kiuchumi.
Aliongeza kuwa mpango wa mikopo ya asilimia 10 umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa makundi maalum, kwa kutoa fursa ya kujenga uchumi imara na kuboresha maisha ya wananchi wa Bukombe.

Comments
Post a Comment