Wananchi kutoka kata mbalimbali, wakiwemo watumishi wa umma katika Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, wameungana kuadhimisha Siku ya Muungano kwa kushiriki mazoezi ya mwili (jogging) yaliyoambatana na hamasa kubwa ya uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
Mazoezi hayo yaliyofanyika leo Aprili 26, 2026, yalianzia katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hadi Viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo, yakiongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya Ally Mketo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, mhadis Mragili.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe Mketo alisema kuwa amani, umoja na mshikamano ni nguzo muhimu katika kujenga jamii imara na yenye maendeleo endelevu.
Alisisitiza kuwa maadhimisho ya Siku ya Muungano yanapaswa kutumika kama jukwaa la kuwakutanisha wananchi, kuimarisha uhusiano na kukuza uzalendo miongoni mwa Watanzania.
“Muungano wetu ni hazina kubwa. Ni wajibu wetu sote kuulinda kwa vitendo kwa kudumisha amani, umoja na kushirikiana katika shughuli za maendeleo,” alisema Mketo.
Aliongeza kuwa ushiriki katika shughuli za pamoja kama mazoezi ya mwili husaidia si tu kuboresha afya, bali pia kuimarisha mahusiano ya kijamii.
“Tunapokutana katika shughuli kama hizi, tunaimarisha siyo tu afya zetu bali pia mahusiano yetu. Umoja wetu ndio nguvu yetu, na amani ndiyo msingi wa maendeleo endelevu,” alisisitiza.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendeleza utamaduni wa kushiriki katika michezo na mazoezi ya mwili, akieleza kuwa afya bora ni rasilimali muhimu katika kujenga taifa lenye nguvu na uchumi imara.
Akizungmza kwaniamba ya washiriki wa tukio hilo Lucas Shitahungula alieleza kufurahishwa na maandalizi mazuri, wakisema yamewapa fursa ya kujumuika, kubadilishana mawazo na kuimarisha mshikamano.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo:“Miaka 62 ya Muungano: Amani, Umoja na Mshikamano ni Msingi wa Maendeleo Endelevu.”

Safi sana
ReplyDelete