Na, Ernest Magashi
Waziri wa Nishati, Deogratius John Ndejembi, amewataka Watanzania kutokuwa na taharuki kuhusu upatikanaji wa mafuta, akisisitiza kuwa nchi ina akiba ya kutosha na hali ya usambazaji iko imara.
Waziri Ndejembi amesema hayo leo Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA), EWURA pamoja na Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), kilicholenga kujadili hali ya upokeaji na usambazaji wa mafuta nchini.
Katika kikao hicho, Waziri Ndejembi ameitaka EWURA kuhakikisha mafuta yote yanayotoka kwenye maghala yanafika kwa walengwa waliokusudiwa na kutumika ipasavyo. Aidha, amehimiza vituo vya mafuta kuuza bidhaa kulingana na mahitaji halisi ya soko ili kuepusha mianya ya upungufu usio wa lazima.
Kwa upande wake, ameuagiza Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha maghala yote makubwa ya usambazaji yanapata mafuta kwa wakati, huku akiitaka taasisi hiyo kuweka mfumo madhubuti wa upangaji wa ratiba ya ushushaji wa mafuta (sequencing) ili kuhakikisha usambazaji unakuwa wa usawa na ufanisi nchini kote.
Waziri Ndejembi pia ameeleza kuwa Serikali imekubaliana kuharakisha zoezi la ushushaji wa meli za mafuta zinazoingia nchini, hususan kwa ajili ya matumizi ya ndani, hatua itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imefanya mazungumzo na TIPER ili kuweka utaratibu bora wa upangaji wa ushushaji wa mafuta, utakaowezesha wasambazaji wote kupata huduma kwa haki na kwa wakati.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Mohamed Mohamed pamoja na wataalam mbalimbali wa sekta ya mafuta.

Comments
Post a Comment