WAZIRI WA NISHATI AAGIZA TPDC KUONGEZA KASI YA UPATIKANAJI WA MAENEO MAPYA YA UCHIMBAJI WA GESI


Na, Ernest Magashi

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) kuongeza kasi ya utafiti na upatikanaji wa maeneo mapya ya uchimbaji wa visima vya gesi asilia ili kuimarisha uzalishaji na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati safi nchini.Waziri Ndejembi ametoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara, alipokwenda kuzindua mradi wa uchimbaji wa visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay. Visima viwili ni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa gesi asilia, huku kimoja kikiwa cha utafutaji (exploration). Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 58.“Rai yangu kwa TPDC ni kuongeza kasi ya uchimbaji wa gesi katika maeneo mengine na kuhakikisha mashapo yaliyothibitika yanaanza kuzalisha mapema. Tunapozindua kitalu hiki, mipango ya kuanza uchimbaji katika maeneo mengine ianze mara moja,” amesema Ndejembi.Ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuwekeza fedha kupitia TPDC ili kuimarisha sekta ya gesi, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati kadri uchumi wa nchi unavyokua. Mahitaji hayo yanatokana na uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani na taasisi, nishati kwa vyombo vya usafiri pamoja na matumizi ya majumbani.Waziri huyo pia ameipongeza TPDC kwa kushirikiana na Kampuni ya Maurel & Prom katika utekelezaji wa mradi huo, akisema utaongeza uzalishaji wa gesi na kuchochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Taifa.Aidha, ameisisitiza TPDC kuendelea kuyawezesha makampuni na wataalamu wazawa kwa kuwajengea uwezo na kuwashirikisha kikamilifu katika miradi ya gesi, ili wanufaike na rasilimali za nchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 235 katika mradi huo, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha sekta ya gesi nchini.Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, amesema Serikali kupitia TPDC inamiliki asilimia 40 ya hisa katika Kitalu cha Mnazi Bay, huku Maurel & Prom ikimiliki asilimia 60. Amebainisha kuwa uzalishaji katika kitalu hicho umefikia futi za ujazo milioni 100 za gesi kwa siku, hatua inayodhihirisha mafanikio ya uwekezaji huo.

Comments