WAZIRI MKUU AAGIZA MAPATO YA NDANI YA HALMASHAURI KULIPA WALIMU WANAOJITOLEA

Na, Ernest Magashi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba, ameziagiza halmashauri zote nchini kutumia mapato yao ya ndani kulipa walimu wanaojitolea katika shule mbalimbali badala ya jukumu hilo kubebwa na wazazi.Agizo hilo alilitoa Jumamosi, Machi 14, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Kibaoni, Kata ya Kibaoni, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi, akiwa katika ziara ya kikazi.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisema halmashauri zina uwezo wa kutumia sehemu ya mapato yao ya ndani kusaidia kugharamia malipo ya walimu wanaojitolea, hasa katika maeneo yenye upungufu wa walimu.Alisisitiza kuwa si sahihi jukumu la kuwalipa walimu hao kubebwa na wazazi pekee.

“Serikali hatupaswi kuwabebesha wazazi jukumu la kulipa walimu wanaojitolea. Halmashauri zina mapato ya ndani ambayo yanaweza kutumika kusaidia kulipa walimu hao pale kunapokuwa na uhitaji wa ziada ya walimu,” alisema Dkt. Nchemba.Aidha, aliwahimiza wazazi na walezi kuendelea kushiriki katika maendeleo ya elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata mahitaji muhimu ikiwemo chakula wakiwa shuleni, ili kuwawezesha kusoma katika mazingira bora. Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, halmashauri, wazazi na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.


Comments