WATOA HUDUMA WA AFYA WAPATIWA MAFUNZO YA CHANJO YA MATONE YA POLIO (nOPV2)


Na, Ernest Magashi

Watoa huduma za afya kutoka Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamepatiwa mafunzo maalum ya utoaji wa chanjo ya matone ya polio (nOPV2), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kampeni ya kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa polio.Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu hao ili waweze kutoa huduma bora, salama na yenye ufanisi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10 katika maeneo yao ya kazi.Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Deograsia Mkapa, aliwataka washiriki kuzingatia weledi, umakini na ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kampeni ya chanjo inafanikiwa.Alisisitiza kuwa mafanikio ya kampeni hiyo yanategemea nidhamu ya kazi, mawasiliano sahihi pamoja na utoaji wa taarifa kwa wakati, akibainisha kuwa kila mtoa huduma ana jukumu muhimu katika kulinda afya ya jamii.Dkt. Mkapa alieleza kuwa chanjo ya polio ni kinga madhubuti dhidi ya ulemavu unaoweza kuzuilika, hivyo wataalamu wanapaswa kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa huduma hiyo.Aidha, aliwahimiza watoa huduma kuwa mabalozi wazuri kwa jamii kwa kutoa elimu sahihi kuhusu umuhimu wa chanjo, ili kuondoa dhana potofu na kuongeza mwitikio wa wananchi.Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa kampeni ya chanjo ya polio wilayani Bukombe, pamoja na kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa watoa huduma za afya.Hatua hii ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhakikisha kila mtoto analindwa dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, na hivyo kujenga jamii yenye afya bora na nguvu kazi imara kwa maendeleo endelevu.

Comments