Wanawake wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameaswa kuendelea kuimarisha malezi ya kimaadili kwa watoto kwa kuzingatia mila, desturi na tamaduni za Kitanzania ili kukuza jamii yenye maadili mema kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, wakati akihutubia wanawake katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika leo kiwilaya Machi 5, 2026 katika uwanja wa CCM, Kata ya Igulwa, wilayani Bukombe.
Dkt. Biteko alisema wanawake wana nafasi kubwa katika malezi ya watoto na kujenga msingi wa taifa lenye maadili bora, hivyo hawapaswi kupunguza juhudi katika kuwalea watoto bila ubaguzi ili kuhakikisha taifa linapata viongozi bora wa baadaye.
Alisema malezi bora yatawezesha taifa kupata viongozi wazalendo na wenye maadili mema kama ilivyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha aliwataka wanaume kutekeleza wajibu wao katika familia kwa kuwaheshimu na kuwathamini wanawake ambao wanabeba jukumu kubwa la kulea familia pamoja na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
“Wanaume tujinyime, tuvumiliane na tuishi kwa upendo katika familia. Tuwathamini watoto wa kike na wanawake kwa sababu nao wana uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo kama ilivyo kwa wanaume,” alisema Dkt. Biteko.
Aliahidi kuendelea kushirikiana na wanawake wa Wilaya ya Bukombe katika kuwawezesha kiuchumi na kuipongeza Halmashauri kwa kuendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake.
Pia aliwahimiza wanawake kutumia kikamilifu fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza kipato cha familia pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Bukombe, Annastera Athanas, akisoma risala ya wanawake, aliiomba Serikali kuendelea kudhibiti vitendo vya mmomonyoko wa maadili, ikiwemo biashara ya ngono ambayo imekuwa chanzo cha kuenea kwa magonjwa hatari yakiwemo maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwataka wanawake kuendelea kushirikiana na waume zao katika kujenga familia imara hata pale wanapofanikiwa kiuchumi.
Alisema halmashauri inatarajia kutoa mikopo katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha, hivyo aliwahimiza wanawake kutumia fursa hiyo ili kuendelea kunufaika na sera za uwezeshaji wa kiuchumi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Comments
Post a Comment