Wanawake waumini wa Kanisa la Ufunuo Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Ufunuo Jimbo la Geita, Rosemeri Mashauri, wametembelea Gereza la Wanawake Wilaya ya Kahama na kutoa msaada wa matendo ya huruma kwa wafungwa wanawake walioko katika gereza hilo.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8. Kwa mwaka 2026, maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha "Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya 2050”
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Askofu Mashauri aliwapongeza askari wa Jeshi la Magereza kwa namna wanavyoendelea kuwahudumia wafungwa kwa upendo na utu. Pongezi hizo zilifuata baada ya msafara wa wanawake hao kupokelewa kwa heshima na askari wa gereza hilo.
Katika ziara hiyo, Askofu Mashauri pamoja na waumini wa kanisa hilo walikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa wanawake walioko gerezani, ikiwa ni pamoja na sabuni na mahitaji mengine muhimu kwa wanawake pamoja na watoto wanaoishi na mama zao gerezani.
Akizungumza na wafungwa hao wa kike, Askofu Mashauri aliwatia moyo kwa kuwaombea kwa Mungu ili awape uvumilivu, nguvu na tumaini wakati wanapotumikia vifungo vyao kwa mujibu wa sheria.
Aliwaomba kuwa na matumaini kwamba ipo siku watamaliza adhabu zao na kurejea uraiani wakiwa raia wema na wenye mchango chanya katika maendeleo ya jamii.
Katika ziara hiyo pia, Askofu Mashauri aliwasilisha salamu za Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Doto Biteko, akieleza kuwa anawajali na kuwathamini huku akiwataka kuwa na subira na matumaini kwani kipindi wanachopitia ni sehemu ya changamoto za maisha.
Kwa upande wake, uongozi wa Gereza la Wanawake Wilaya ya Kahama uliwashukuru wanawake wa Kanisa la Ufunuo kwa kuwafikia wafungwa hao na kuwafariji, ukisema msaada walioutoa utasaidia kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu ya wafungwa hao.
Aidha, Mkuu wa Gereza Wilaya ya Bukombe Patrick mandago aliwahimiza kuendelea kudumisha moyo wa kujitolea kwa kuwatembelea na kuwafariji watu wenye uhitaji, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kuwapa faraja na matumaini wafungwa walioko gerezani.
Katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani yaliyofanyika kiwilaya Machi 5, 2026 katika Wilaya ya Bukombe, Dkt. Biteko ambaye alikuwa mgeni rasmi aliahidi kuendelea kushirikiana na wanawake wa wilaya hiyo katika kuimarisha harakati zao za kiuchumi ili waweze kujitegemea na kuchangia zaidi maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mbunge huyo alisema wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii, hivyo ni muhimu kuendelea kuwaunga mkono katika shughuli zao za kiuchumi ikiwemo biashara ndogo ndogo, vikundi vya ujasiriamali na shughuli nyingine za maendeleo.

Comments
Post a Comment