WANANCHI WAMFAGILIA DKT. BITEKO KWA UTEKELEZAJI WA AHADI YA UJENZI WA DARAJA


Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Kata ya Bugelenga, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Doto Biteko, kwa kusimamia na kufanikisha utekelezaji wa ahadi yake ujenzi wa Daraja la Bugelenga linalounganisha Wilaya za Bukombe na Mbogwe.Pongezi hizo zimetolewa na wananchi Jocy Tobias na Shija Migata walipozungumza na mwandishi wa habari, wakieleza furaha yao kuona mradi huo ukiendelea kutekelezwa.Walisema daraja hilo litafungua fursa mpya za kiuchumi na kurahisisha usafirishaji wa mazao pamoja na mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili.Tobias alieleza kuwa kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakipata changamoto ya kuvusha mazao yao wakati wa mvua za masika, hali iliyowalazimu kuzunguka kupitia jijiji cha Mwalo, Lyambamgongo na Bukombe ili kufika Masumbwe, Wilaya ya Mbogwe. Alisema kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza gharama na muda wa usafiri, hivyo kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi.Kwa upande wake, Migata alisema Dkt. Biteko kwa kushirikiana na Serikali amekuwa mstari wa mbele kusukuma miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa daraja hilo ni miongoni mwa miradi iliyogusa moja kwa moja maisha ya wananchi kwa kutatua kero ya muda mrefu ya usafirishaji  wa biashara.Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkange, Timbola Kasungwa, aliipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi huo, akisema ukikamilika utaongeza mzunguko wa biashara katika vijiji vya mpakani na kukuza kipato cha wananchi mmoja mmoja pamoja na Taifa kwa ujumla.Akizungumza hivi karibuni wakati wa ziara ya kukagua mradi huo, Diwani wa Kata ya Bugelenga, Donald Lubigisa, alimpongeza Mbunge huyo kwa kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha daraja linajengwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma katika wilaya jirani.Lubigisa alisema mradi huo umegharimu Shilingi milioni 583.83 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia maombi yaliyowasilishwa na Mbunge baada ya kupokea ombi kutoka kwa diwani na wananchi.Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Msoka Msumba, alisema ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa. Alibainisha kuwa daraja hilo lenye urefu wa mita 60.54 ni miongoni mwa madaraja marefu ya mawe katika Mkoa wa Geita, na kwamba litachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha miundombinu ya usafiri katika eneo hilo.

Comments