Wananchi wa Kata ya Bukombe mkoani Geita wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa juhudi zake za kuchangia na kusimamia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ituga unaoendelea katika eneo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walieleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo, wakisema utakapokamilika utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hicho na maeneo jirani.
Amos Daud, mkazi wa Kata ya Bukombe, alisema zahanati hiyo itakuwa mkombozi kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
“Tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Biteko kwa kutusogezea huduma muhimu ya afya. Zahanati hii itarahisisha upatikanaji wa matibabu na kuokoa muda na gharama za wananchi,” alisema Amos.
Naye Neema Paul alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya mbunge huyo katika kuwaletea wananchi maendeleo, hususan katika sekta ya afya.
“Hii ni ishara kwamba kiongozi wetu anajali mahitaji ya wananchi wake. Tuna imani zahanati hii itakapokamilika itaboresha huduma za afya, hasa kwa kina mama na watoto,” alisema Neema.
Wakati wa ziara yake katika kata hiyo, Dkt. Biteko alianza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Dkt. Biteko kupitia mkutano huo, aliwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta tija kwa jamii.
Aidha, alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi, huku akiahidi kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kijamii katika Jimbo la Bukombe

Comments
Post a Comment