WANAFUNZI WA KIKE BUKOMBE WAPONGEZWA KWA UFAULU WA MASOMO


Na, Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, amewapongeza wanafunzi wa kike wa wilaya hiyo kwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya kitaaluma ya mwaka 2025/2026.Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika ngazi ya wilaya Machi 5, 2026 katika mji wa Ushirombo, Kata ya Igulwa, ambapo alieleza kuwa ufaulu wa wanafunzi wa kike ni ishara ya juhudi kubwa zinazofanywa na walimu pamoja na wanafunzi wenyewe.

Alisema mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu ya wanafunzi wengine kuongeza bidii katika masomo ili kufikia malengo na ndoto zao za baadaye.“Tunajivunia kuona wanafunzi wa kike wakifanya vizuri katika mitihani yao. Hii inaonesha juhudi kubwa zinazofanywa na walimu pamoja na wanafunzi wenyewe. Naomba muendelee kujituma ili kufikia ndoto zenu,” alisema Dkt. Biteko.Aidha, aliwashukuru walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwalea na kuwajenga wanafunzi kitaaluma pamoja na kuwapa ujasiri na kujiamini katika masomo yao.Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko aliahidi kuendelea kushirikiana na wanawake wa Wilaya ya Bukombe katika kuimarisha shughuli zao za kiuchumi ili waweze kujitegemea na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.Alisema wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii, hivyo kuna umuhimu wa kuwawezesha kuanzia kwenye elimu hadi katika shughuli za kiuchumi kama biashara ndogo ndogo, vikundi vya ujasiriamali na shughuli nyingine za maendeleo.

Pia alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazofanya katika kuboresha huduma za afya na elimu nchini, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wanawake.Aidha, aliwataka wananchi wa Bukombe kudumisha upendo, mshikamano na uvumilivu katika familia na jamii ili kujenga mazingira bora ya malezi na maendeleo.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa kike kutoka shule tatu sekondari mbili na shule moja ya msingi walioshiriki katika maadhimisho hayo walisema maneno ya Dkt. Biteko yamewapa motisha ya kuongeza juhudi katika masomo yao ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Comments