WAISLAMU WAMSHUKURU DKT. BITEKO KWA KUANDA IFTARI NA KUENDELEA KUWAUNGANISHA WANANCHI


Na, Ernest Magashi

Waumini wa dini ya Kiislamu katika Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, wamemshukuru Mbunge wa Jimbo hilo, Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kuandaa futari iliyowawezesha kufuturu kwa pamoja, pamoja na juhudi zake za kuendelea kuwaunganisha wananchi bila kujali tofauti zao.Shukrani hizo zilitolewa na Sheikh wa Mkoa wa Geita, Alhaji Alhad Kabaju, katika Uwanja wa Mwenge kata ya Uyovu Machi 16, 2026 wakati wa futari iliyoandaliwa na mbunge huyo. Alisema tukio hilo limekuwa la kudumu tangu Dkt. Biteko alipochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015, na limekuwa likiwaleta pamoja wananchi wa dini mbalimbali.Aliongeza kuwa katika maeneo mengine, matukio ya aina hiyo si ya kawaida, lakini Bukombe imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kutokana na juhudi za mbunge wake. Pia alieleza kuwa hata viongozi wa dini kutoka maeneo mengine, akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, wamelitambua tukio hilo kama la mfano bora wa kuigwa.“Sisi Waislamu tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akupe afya njema na akubariki zaidi Dkt. Biteko, ili uendelee kuwatumikia wananchi wa Bukombe na Watanzania kwa ujumla,” alisema Sheikh Kabaju.Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Hamid Masoud Jongo, kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuendeleza mshikamano kati ya Waislamu na Wakristo, akisema hilo ni agizo la Mungu la kutenda mema na kuishi kwa upendo.Alisema mbunge huyo ni mfano wa uongozi unaojali maendeleo na umoja wa wananchi bila kujali tofauti za kiitikadi au kidini, na kuwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.Aidha, aliwahimiza Waumini wa Kiislamu kuendelea kumuombea mbunge huyo ili Mungu aendelee kumpa afya njema na nguvu ya kuwahudumia wananchi, akibainisha kuwa kitendo cha kuwaalika watu wa dini mbalimbali kwenye futari ni jambo la kupongezwa na lenye thawabu.Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Doto Biteko aliwashukuru wageni wote waliohudhuria, akisema kitendo cha Waislamu kuacha kufuturu majumbani mwao na kushiriki futari ya pamoja ni heshima kubwa kwake na ishara ya mshikamano.Alisema umoja huo ni muhimu katika kujenga jamii yenye nguvu, na kuwashukuru wote waliotoka maeneo mbalimbali kuja kushiriki tukio hilo.Pia aliwahimiza Waumini wa dini ya Kiislamu kuungana na Wakristo kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili Mungu aendelee kumlinda katika kuliongoza taifa.Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani nchini, akibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye utulivu, na kuwataka wananchi kuendelea kuliombea taifa ili amani iendelee kudumu.Aliongeza kuwa viongozi wote, kuanzia ngazi ya juu hadi vijijini, wanahitaji kuombewa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuleta maendeleo kwa wananchi.Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mragili, alisema kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukombe amekuwa na utaratibu wa kuwaunganisha wananchi kupitia matukio mbalimbali ya kijamii yanayoandaliwa na Dkt. Biteko, huku akionyesha jitihada kubwa na kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya wilaya hiyo.


 

Comments