SERIKALI YAONGEZA NGUVU KUHAKIKISHA UPATIKANAJI WA MAFUTA NCHINI

Na, Ernest Magashi

Waziri wa Nishati, Deogratias Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo na wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinazoshughulikia sekta ya mafuta na gesi, katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.Kikao hicho kilichofanyika leo, Machi 28, 2026, ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mafuta nchini, pamoja na kudhibiti athari za mabadiliko ya soko la kimataifa.Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Ndejembi alisisitiza umuhimu wa taasisi hizo kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta na mfumo thabiti wa usambazaji.Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa, changamoto ya uhaba wa mafuta inayojitokeza kwa sasa inachangiwa kwa kiasi kikubwa na misukosuko ya soko la kimataifa, hususan vita vinavyoendelea katika ukanda wa Mashariki ya Kati. Hali hiyo imeathiri njia muhimu za usafirishaji wa mafuta, ikiwemo kupungua kwa upitishaji wa shehena kupitia Strait of Hormuz, jambo lililosababisha ucheleweshaji wa mizigo na kupungua kwa upatikanaji wa mafuta katika baadhi ya maeneo.Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, James Mataragio; Kamishna wa Mafuta na Gesi, Goodluck Shirima; na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, James Mwainyekule.Wengine ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Musa Makame; Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon; pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati.

Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya hali ya upatikanaji wa mafuta nchini, sambamba na kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kukabiliana na changamoto zilizopo.


Comments