REFA ALIYECHEZESHA DERBY YA YANGA NA SIMBA ATEULIWA KOMBE LA DUNIA 2026


Na, Mwandishi Wetu

Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limemteua mwamuzi kutoka Misri, Amin Mohamed Amin Omar, kuwa miongoni mwa waamuzi wa kati watakaochezesha michezo ya Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, 2026.Amin Omar anakumbukwa na mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania baada ya kuchezesha mechi ya ‘Kariakoo Derby’ kati ya Young Africans Sports Club (Yanga) na Simba Sports Club iliyochezwa Juni 25, 2025.Katika mchezo huo, Amin Omar alisaidiwa na waamuzi wasaidizi Mahmoud Ahmed Abo El Regal na Samir Gamal Saad Mohamed, huku Ahmed Mahrous Elghandour akiwa mwamuzi wa akiba. Mtathimini wa mchezo alikuwa Alli Mohamed kutoka Somalia na kamisaa alikuwa Salim Omary Singano kutoka Tanga.Katika derby hiyo, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba. Bao la kwanza lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Pacome Zouzoua dakika ya 66 baada ya kipa Moussa Camara kufanya madhambi, kabla ya Clement Mzize kuongeza bao la pili dakika ya 86.Ushindi huo uliifanya Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/2025 baada ya kumaliza ligi ikiwa na pointi 82, ikicheza mechi 30, kushinda 27, sare moja na kupoteza michezo miwili. Huo ulikuwa ubingwa wa 31 kwa klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965.Mbali na Amin Omar, waamuzi wengine wa kati kutoka Afrika walioteuliwa kuchezesha Kombe la Dunia 2026 ni Dahane Beida kutoka Mauritania, ambaye aliwahi kuchezesha mechi ya Mamelodi Sundowns dhidi ya Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika, pamoja na Mustapha Ghorbal (Algeria), Jean-Jacques Ndala (DR Congo) aliyesimamia fainali ya Africa Cup of Nations 2025, na Pierre Ghislain Atcho kutoka Gabon.

Kwa upande wa teknolojia ya VAR, FIFA imeteua waamuzi Mahmoud Ashour (Misri), Letticia Viana (Eswatini) na Lahlou Benbraham (Algeria).Uteuzi wa waamuzi hao wanane kutoka Afrika unaonesha kuendelea kuongezeka kwa nafasi na mchango wa bara hilo katika kusimamia mashindano makubwa ya soka duniani, huku FIFA ikilenga kuhakikisha ubora na usahihi wa maamuzi katika mechi za Kombe la Dunia 2026.


Comments