REA YATOA ZAIDI YA BILIONI 5.4 KWA MRADI WA UMEME WA MAJI LUPALI


Na, Ernest Magashi

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa zaidi ya shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji katika eneo la Lupali, mkoani Njombe, wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317.Taarifa hiyo imetolewa Machi 11, 2026 wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilipotembelea mradi huo unaotumia maporomoko madogo ya maji ya Mto Lupali kuzalisha umeme.Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, Emmanuel Yessaya, amesema Serikali kupitia REA imetoa ruzuku hiyo kwa awamu tano, yenye jumla ya shilingi bilioni 5.4 ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo.Yessaya amesema mradi huo unatekelezwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha, ambalo linaendesha shughuli za maendeleo katika eneo hilo.Ameeleza kuwa fedha zilizotolewa na REA zimewezesha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme pamoja na miundombinu ya kusambaza umeme katika kituo cha Imiliwaha Sisters Convent na vijiji vya jirani vya Boimanda, Kitulila na Matola, sambamba na kufanikisha tafiti za awali za mradi huo.Kwa mujibu wa Yessaya, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99, ambapo kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, ameipongeza REA kwa kuwekeza fedha nyingi katika mradi huo, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe.Naye Mratibu wa mradi huo, Sista Imakulata Mlowe, amesema baada ya mradi kukamilika umeme utakaotokana na kituo hicho utauzwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), huku mkataba wa mauziano ya umeme ukiwa tayari umeshasainiwa.Ameongeza kuwa mradi huo utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za kiuchumi, sambamba na kupunguza matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira.Ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) mkoani Njombe imelenga kujionea utekelezaji wa miradi ya REA pamoja na kufuatilia maendeleo ya waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme nchini ili kubaini changamoto na kutafuta ufumbuzi wake.

Comments