Katika kina cha bahari zenye baridi kali za kaskazini, anaishi mnyama wa ajabu anayevunja mipaka ya uhai wa viumbe duniani. Mnyama huyo ni Greenland shark, papa anayesifika kwa kuishi kwa muda mrefu zaidi kuliko mnyama yeyote mwenye uti wa mgongo.
Kwa mujibu wa tafiti za kisayansi zilizofanywa na watafiti kama Julius Nielsen kutoka University of Copenhagen kwa kushirikiana na Jan Heinemeier, papa huyu ana uwezo wa kuishi kati ya miaka 250 hadi 400, huku baadhi yao wakikadiriwa kuzidi hata umri huo.Hii ina maana kuwa baadhi ya papa wanaoishi leo huenda walizaliwa karne nyingi zilizopita.
Kwa mfano, wanasayansi hao walichunguza papa mmoja aliyekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 390 kwa kutumia mbinu ya kisasa ya kupima umri wa tishu za macho. Ugunduzi huu uliweka rekodi mpya ya mnyama mwenye uti wa mgongo anayeishi muda mrefu zaidi duniani.
Papa huyu hupatikana katika bahari za baridi kali za eneo la Arctic pamoja na kaskazini mwa Bahari ya Atlantic. Maji haya yenye joto la chini huchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza muda wa maisha yake.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, maisha marefu ya papa huyu yanatokana na mambo kadhaa, ikiwemo:
Ukuaji wake kuwa wa polepole sana Mwili wake kufanya kazi kwa utaratibu wa taratibu (slow metabolism) Kuishi katika mazingira ya baridi kali yasiyobadilika haraka Cha kushangaza zaidi ni kwamba papa huyu huchukua takribani miaka 100 hadi 150 kufikia umri wa kuzaa, jambo linaloonesha namna anavyokua taratibu sana.
Jinsi umri wake unavyopimwa Tofauti na wanyama wengine, papa wa Greenland hana mifupa inayorahisisha kupima umri wake. Badala yake, watafiti kama Jan Heinemeier walitumia mbinu ya kuchunguza tishu za macho kwa kutumia teknolojia ya radiocarbon dating ili kubaini umri wake halisi.
Maumbile na tabia, Papa huyu anaweza kufikia urefu wa mita 5 hadi 7 na uzito mkubwa. Licha ya ukubwa wake, anasifika kwa mwendo wa polepole, lakini ni mwindaji mwenye ustadi wa kuvizia mawindo yake kimyakimya.
Pamoja na uimara wake wa kuishi muda mrefu, anakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuvuliwa kwa bahati mbaya kwenye nyavu za uvuvi pamoja na kuzaliana polepole, hali inayofanya idadi yao kuongezeka kwa taratibu sana.
Kwa ujumla, Greenland shark ni miongoni mwa maajabu makubwa ya viumbe hai duniani. Uwezo wake wa kuishi kwa karne nyingi unaendelea kuwashangaza wanasayansi na kutoa funzo kuwa mazingira na mfumo wa maisha vina mchango mkubwa katika urefu wa uhai.
Mnyama huyu anaendelea kubaki kuwa siri kubwa ya bahari, huku tafiti zaidi zikiendelea kufanyika ili kufahamu kwa undani zaidi maisha yake ya kipekee.


Comments
Post a Comment