Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amekabidhi vitendea kazi vya usafiri kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga, ikiwa ni jitihada za kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kutatua changamoto za wateja kwa haraka.
Akizungumza Machi 27, 2026 katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Makamba alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika na kwa wakati.
Alisema vitendea kazi hivyo vitaongeza ufanisi kwa watumishi wa TANESCO mkoani humo na kuwawezesha kuwafikia wateja kwa haraka zaidi pamoja na kutatua changamoto zao kwa wakati.
“Kupitia vyombo hivi vya usafiri, tutaleta mabadiliko makubwa katika kuwafikia wateja na kuwahudumia kwa ufanisi. Niwaombe vitumike ipasavyo kutatua changamoto za wananchi kwa wakati,” alisema Makamba.
Aidha, Makamba alitumia fursa hiyo kuhamasisha wakazi wa Kahama, hususan wanawake, kutumia nishati safi ya umeme kupikia, akieleza kuwa ni nafuu, salama na rafiki kwa mazingira.
“Niwaombe wakina mama wa Kahama tuchangamkie matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme. TANESCO wameleta majiko ya umeme ambayo yanarahisisha upishi na kuokoa muda,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, alisema Serikali kupitia TANESCO inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Manispaa ya Kahama, akibainisha kuwa zaidi ya shilingi milioni 600 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa laini mpya za umeme zitakazohudumia wakazi wa eneo hilo, sambamba na ukuaji wa mji huo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Benson Mbigili, alisema wamepokea vitendea kazi mbalimbali vikiwemo magari manne, bajaji moja na pikipiki nne.
Mbigili aliipongeza Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo, akisema vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia wateja, hususan katika maeneo yenye changamoto ya miundombinu.
“Magari haya yatatuwezesha kuwafikia wateja wapya hata katika maeneo korofi ambayo awali ilikuwa vigumu kufikika. Tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora na ya uhakika,” alisema Mbigili.
Aliongeza kuwa TANESCO Mkoa wa Shinyanga inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme ili kuongeza uelewa wa wananchi juu ya faida zake kiuchumi na kimazingira.

Comments
Post a Comment