Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia kijana mmoja, Ibrahimu Kitundu (18), mkazi wa Kata ya Ipuli, kwa tuhuma za kufanya shambulio la kijinsia dhidi ya mtoto mdogo, tukio linalodaiwa kuchochewa na imani za kishirikina.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilijiri Machi 22, 2026 majira ya saa sita mchana katika Mtaa wa Nyerere, Manispaa ya Tabora.
Kwa mujibu wa Kamanda Abwao, mtuhumiwa anadaiwa kumchukua mtoto huyo kutoka nyumbani kwao na kumpeleka katika kibanda kilichopo jirani na eneo hilo, ambapo alifanya kitendo hicho cha kinyume na maadili.
Alisema baada ya tukio hilo, wananchi waliokuwa jirani walimtia shaka mtuhumiwa na kuamua kumfuatilia, ndipo walipomkuta mtoto huyo akiwa katika hali mbaya kiafya.
Katika mahojiano ya awali, mtuhumiwa amekiri kutenda kitendo hicho na kudai kuwa alishawishiwa na mtuanayehusishwa na kikundi cha sanaa cha Nyanyembe Film, akieleza kuwa walifuata masharti waliyopewa na mganga wa jadi ili kupata mafanikio katika kazi zao za filamu.
Kamanda Abwao alibainisha kuwa chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na imani potofu za kishirikina, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kuwabaini watu wengine waliohusika.
Amesema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na hatua za kisheria dhidi yake zinaendelea kuchukuliwa.

Comments
Post a Comment