Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita limesema hadi sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kufariki dunia kufuatia tukio la kifusi cha udongo kuporomoka katika Mgodi wa Msasa Gold Mine uliopo Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 30, 2026 eneo la tukio, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Keneth Mwakasitu, alisema zoezi la utafutaji linaendelea licha ya kutopatikana kwa mwili wa mtu yeyote tangu tukio hilo litokee.
Alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Machi 29, 2026 majira ya saa 4:30 asubuhi, baada ya maeneo ya maduwala manne yaliyokuwa yamesimamishwa kwa ajili ya ukarabati kuonyesha dalili za hatari, hatua iliyosababisha watu kuondolewa mapema kwa tahadhari.
“Nilipigiwa simu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Sofia Jongo, akinijulisha kuhusu tukio hilo. Timu ya zimamoto wilaya ilifika haraka na kubaini kuwa baadhi ya mashimo yalikuwa yameporomoka, lakini kwa bahati nzuri hapakuwa na mtu yeyote ndani ya eneo hilo,” alisema Mwakasitu.
Aliongeza kuwa zoezi la utafutaji lilihusisha vyombo mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi, wataalamu wa mgodi pamoja na uongozi wa mgodi huo, ambapo hadi saa 5:00 usiku wa Machi 29, 2026 walilazimika kusitisha shughuli hiyo kwa muda bila mafanikio ya kubaini uwepo wa binadamu yeyote.
Kamanda Mwakasitu pia alikemea vikali kusambazwa kwa taarifa zisizo sahihi mitandaoni zinazodai kuwepo kwa watu waliopoteza maisha au kufukiwa na kifusi.
“Wananchi wanapaswa kupuuza taarifa za uzushi. Hadi sasa hakuna mwili wa binadamu wala kiumbe chochote kilichopatikana. Tutaendelea na utafutaji pamoja na hatua za kiusalama kuhakikisha eneo ni salama kabisa,” alisisitiza.
Aidha, alisema shughuli zote za uchimbaji katika maduwala mgidini hapo zimesimamishwa kwa muda ili kupisha tathmini ya kina ya usalama, akibainisha kuwa kipaumbele chao ni kulinda maisha ya watu kabla ya kuendelea na uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Mgodi huo, James Balele malufu mwana Nkamba, alisema waligundua dalili za nyufa katika eneo hilo Machi 28, 2026 na kutoa maelekezo ya kusitisha shughuli pamoja na kuanza ukarabati.
Balele alisema kabla ya tukio, eneo hilo lilikuwa limewekewa alama za tahadhari na kufungwa ili kuzuia watu kuingia, na kwamba Machi 29, 2026 walibaini nyufa zimeongezeka na kuamua kuwaondoa watu wote waliokuwa karibu.
“Dakika chache baada ya kuwaondoa watu, ndipo eneo hilo liliporomoka. Hakukuwa na mtu ndani ya maduwala wala juu ya eneo hilo,” alisema Balele.
Mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo fundi katika mgodi huo, Shukulu Kapela, alithibitisha kuwa wakati tukio linatokea hapakuwa na mtu yeyote eneo hilo, akisisitiza kuwa taarifa za vifo ni za uongo.
Naye mtaalamu wa ulipuaji miamba (blaster), Ngwesa Masuka, alisema kuporomoka huko kulisababishwa na mmomonyoko wa udongo, na kusisitiza kuwa tahadhari zilizochukuliwa zilisaidia kuokoa maisha ya watu.

Comments
Post a Comment