Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Sofia Jongo, ameendesha mkutano wa hadhara katika eneo la Mgodi wa Msasa Gold Mine kwa lengo la kuhakiki taarifa za kuwepo kwa watu wanaodaiwa kufukiwa na udongo kufuatia kuporomoka kwa mashimo (duwala) katika mgodi huo.
Akizungumza mbele ya wananchi na wachimbaji, Kamanda Jongo aliwataka watu wote kuwa wakweli na kujitokeza iwapo kuna mtu yeyote aliyepoteza ndugu au rafiki katika tukio hilo, ili Serikali iweze kuchukua hatua stahiki.
Mkutano huo umefanyika wakati vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, vikiwa katika siku ya tatu ya zoezi la uokoaji na utafutaji katika eneo la duwala nne zilizoporomoka, bila mafanikio ya kubaini mwili wa binadamu hasi sasa.
Katika mkutano huo, wananchi na wachimbaji waliombwa kunyosha mikono iwapo kuna aliyefiwa, lakini hakuna hata mmoja aliyejitokeza, hali iliyomfanya Kamanda Jongo kusisitiza mara kadhaa ili kuhakikisha ukweli wa taarifa hizo.
Wananchi walijibu kwa pamoja wakisema hakuna mtu aliyefariki au kufukiwa, hakuna aliyekuwa ndani wakati wa tukio.
“Nimefika hapa Msasa na kuitisha mkutano huu ili kuhakikisha kama kuna mtu yeyote aliyepoteza ndugu au rafiki ajitokeze hadharani, lakini mpaka sasa hakuna aliyeripoti kupoteza mtu,” alisema Kamanda Jongo.
Aliongeza kuwa taarifa za vifo zinazozungumzwa mitandaoni ni za upotoshaji na huenda zinatokana na watu wenye nia ya kudhoofisha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda Jongo, tangu Machi 29, 2026, juhudi za utafutaji zimeendelea kufanyika bila kubaini dalili zozote za uwepo wa mwili wa binadamu, hali inayoashiria kuwa hakuna aliyepata madhara.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Kenneth Mwakasitu, alisema kuwa tangu kuanza kwa operesheni hiyo, hakuna ushahidi wa mtu aliyenaswa ndani ya mashimo hayo.
Naye Mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Mgodi huo, James Balele, maarufu kama Mwana Nkamba, alieleza kuwa kabla ya tukio hilo, eneo hilo lilikuwa tayari limebainika kuwa na hatari ya kuporomoka, na wachimbaji waliondolewa mapema kwa tahadhari.
Alifafanua kuwa wakati tukio linatokea majira ya saa 4:30 asubuhi, hakukuwa na mtu ndani ya mashimo hayo, isipokuwa baadhi ya vifaa vya uchimbaji vilivyokuwa juu ya eneo hilo kama jenereta, winchi na pampu za maji.
Aidha, mchimbaji mmoja, Charles John, aliomba Serikali iruhusu kuendelea kwa shughuli za uchimbaji katika maeneo salama, akieleza kuwa wachimbaji wana imani kuwa hakuna mtu aliyefariki wala kujeruhiwa.
Akijibu ombi hilo, Kamanda Jongo alisema atalichukua na kulifanyia kazi baada ya kukamilika kwa tathmini ya usalama katika eneo hilo.

Comments
Post a Comment