JESHI LA POLISI LAFUTA MAADHIMISHO YA BAWACHA MUSOMA


Na, Ernest Magashi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limezuia kufanyika kwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyokuwa yamepangwa kufanywa Machi 8, 2026 mjini Musoma na Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA).

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amesema hatua hiyo inatekeleza amri ya mahakama inayokataza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanya shughuli za kisiasa hadi shauri la msingi linalowakabili litakapomalizika mahakamani.Kamanda Lutumo amesema Jeshi la Polisi lilipitia taarifa na picha zilizosambazwa kupitia mitandao ya kijamii zikionyesha maandalizi na uhamasishaji wa maadhimisho hayo, jambo alilosema ni ukiukwaji wa makusudi wa amri ya mahakama ambayo bado iko hai na haijatenguliwa.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limewataka viongozi wa BAWACHA waliohusika na kikao cha maandalizi kufika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mara (Makosa ya Jinai) tarehe 2 Machi 2026 kwa ajili ya mahojiano.“Jeshi la Polisi linaendelea kuheshimu na kutekeleza amri ya mahakama kwa kuwa haijatenguliwa. Tunawashauri CHADEMA kurejea mahakamani kumaliza shauri lao badala ya kukaidi amri hiyo, kwani kufanya hivyo ni sawa na dharau kwa mahakama (contempt of court),” amesema Lutumo.

Jeshi hilo limewahimiza wananchi kuendelea kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa ili kulinda amani na utulivu wa Mkoa wa Mara na nchi kwa ujumla

Comments