DKT. SAMIA SULUHU HASSAN NI KIONGOZI BORA MWANAMKE BARANI AFRIKA, DKT. BITEKO


Na, Ernest Magashi

Wanawake na wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametakiwa kumtambua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuwa ni miongoni mwa viongozi bora wanawake barani Afrika kutokana na uongozi wake thabiti na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, wakati akizungumza na wanawake wa Wilaya ya Bukombe katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani yaliyofanyika ngazi ya wilaya Machi 5, 2026 katika uwanja wa CCM uliopo Kata ya Igulwa.Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Biteko alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi tangu alipoingia madarakani, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa viongozi wanawake bora barani Afrika. Alieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na usimamizi wake wa miradi mikubwa ya maendeleo ya kiuchumi pamoja na kuhimiza misingi ya utawala bora nchini.Dkt. Biteko aliwataka baadhi ya watu katika jamii kuacha tabia ya kumdharau mwanamke, akisisitiza kuwa uwezo na uimara wa Rais Samia ni mfano tosha unaoonyesha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kuongoza na kuleta maendeleo.Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana na wanawake wa Wilaya ya Bukombe katika kuimarisha harakati zao za kiuchumi ili waweze kujitegemea na kuchangia zaidi maendeleo ya familia zao pamoja na taifa kwa ujumla.Akizungumza zaidi katika maadhimisho hayo, Mbunge huyo alisisitiza kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii, hivyo ni muhimu kuendelea kuwaunga mkono katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo biashara ndogo ndogo, vikundi vya ujasiriamali na shughuli nyingine za maendeleo.Pia aliwapongeza wanafunzi wa kike wa Wilaya ya Bukombe kwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya kitaaluma, huku akiwashukuru walimu kwa juhudi zao za kuwajenga wanafunzi hao kitaaluma na kuwapa kujiamini katika masomo yao.“Tunajivunia kuona wanafunzi wa kike wakifanya vizuri katika mitihani. Hii inaonesha juhudi kubwa zinazofanywa na walimu pamoja na wanafunzi wenyewe. Niwaombe muendelee kujituma ili kufikia ndoto zenu,” alisema Dkt. Biteko.Katika hotuba yake, Dkt. Biteko pia aliwahimiza wananchi wa Bukombe kudumisha upendo, mshikamano na kuvumiliana ndani ya familia na jamii ili kujenga mazingira bora ya malezi na maendeleo.Alisisitiza kuwa familia imara hujengwa kwa msingi wa upendo na ushirikiano, hivyo aliwataka wanaume kuwathamini wanawake na kuwasaidia katika majukumu ya nyumbani.“Baba unaposherehekea siku hii ya wanawake, mpunguzie mama kazi hata moja. Mpe sapraizi kwa kumpikia chakula ili naye ajisikie kuthaminiwa,” alisisitiza Dkt. Biteko.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wilaya ya Bukombe, Retisia Molisi, akitoa neno la shukrani alisema Dkt. Biteko amekuwa kiungo muhimu katika kuwasaidia wanawake kupata fursa mbalimbali za kiuchumi wilayani humo.Aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mwanamke shujaa kwa kuwasimamia wananchi na kuwaletea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutoa fursa za mikopo isiyo na riba kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia halmashauri. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwahimiza wanawake kuendelea kutafuta na kutumia fursa za kiuchumi zinazotolewa na halmashauri, akibainisha kuwa halmashauri itaendelea kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.

Comments