DKT. BITEKO AWAALIKA WANANCHI KATIKA IFTARI

Na, Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Naibu Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Doto Biteko, amewaalika wananchi wa Wilaya ya Bukombe pamoja na Watanzania wengine kuhudhuria hafla ya iftari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge Dkt. Biteko, hafla hiyo ya iftari inatarajiwa kufanyika Machi 16, 2026 katika Uwanja wa Mwenge, Kata ya Uyovu, kuanzia majira ya saa 1:00 usiku.Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwaliko huo ni mwendelezo wa utaratibu ulioanzishwa na Mbunge Dkt. Biteko tangu mwaka 2016, ambapo kila mwaka amekuwa akiwakutanisha waumini wa dini ya Kiislamu kwa ajili ya futari katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Imeelezwa kuwa hafla hiyo huwakutanisha waumini kutoka kata zote 17 zinazounda Wilaya ya Bukombe, huku wengine wakitoka katika wilaya jirani kushiriki futari hiyo ya pamoja.Lengo la tukio hilo ni kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya jamii pamoja na kushiriki na waumini wa Kiislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kuelekea Sikukuu ya Eid.

Aidha, hafla hiyo imekuwa pia ikiwakutanisha watu wa makundi mbalimbali ya kijamii kutoka Bukombe na maeneo mengine ya Tanzania, hivyo kutoa fursa ya kuimarisha mahusiano na umoja miongoni mwa wananchi.Kwa nyakati tofauti, wananchi wa Bukombe wamekuwa wakimpongeza Mbunge Dkt. Biteko kwa kuendelea kuandaa futari hiyo kila mwaka, huku wengi wakiahidi kujitokeza kwa wingi kushiriki hafla hiyo. 

Comments