Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, na Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, amewapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa wataalamu wa afya katika zoezi la utoaji wa chanjo ya matone ya Polio, hatua iliyowezesha kuvukwa kwa malengo yaliyowekwa.
Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo kufuatia taarifa ya mafanikio iliyotolewa na Msimamizi wa Chanjo ya Matone ya Polio kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Stephen Mwaisobwa, ambaye aliwapongeza wasimamizi na watoa huduma za afya kwa juhudi na weledi wao katika kufanikisha zoezi hilo.
“Naishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali Watanzania kupitia huduma bora za afya, ikiwemo chanjo zinazotolewa kwa watoto,” alisema Dkt. Biteko.
Alibainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe imefanikiwa kuvuka lengo la utoaji wa chanjo hiyo, baada ya kuchanja watoto 189,253 dhidi ya lengo la watoto 156,777, sawa na utekelezaji wa asilimia 120.7.
Baadhi ya wananchi wameeleza kuridhishwa na zoezi hilo, wakisema elimu iliyotolewa na wataalamu wa afya imechangia kuongeza uelewa na mwitikio wa jamii.
Mkazi wa Bulega, Katalina James, alisema alipeleka watoto wake kupata chanjo kutokana na hamasa na elimu waliyopewa, jambo lililochangia kufikiwa kwa malengo ya Serikali.
Naye mkazi wa Kata ya Ng’anzo, Kilistina Lukas, aliishukuru Serikali akisema ana imani kuwa watoto wake wako salama baada ya kupata chanjo hiyo ya kuwakinga dhidi ya polio.
Mafanikio hayo yanaendelea kuonyesha jitihada za Serikali na wadau wa afya katika kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo, na kuifanya Tanzania kuendelea kubaki salama dhidi ya polio.


Comments
Post a Comment