DC KUKUTANA NA WAKULIMA WA ZAO LA KOROSHO BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Mragili, ameahidi kuitisha kikao maalum kitakachowakutanisha wakulima na wafanyabiashara wa zao la korosho, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha uzalishaji na kukuza uchumi wa wananchi.Ahadi hiyo aliitoa wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kata ya Naminge, alipowatembelea wakulima wa korosho katika Kijiji cha Bugenge. Ziara hiyo iliyofanyika Machi 19, 2026, ilihusisha pia ukaguzi wa mashamba ya korosho pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika Kata ya Runzewe Magharibi.

Akiwa shambani, Mhandisi Mragili alipata fursa ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wakulima, ambapo walieleza changamoto zinazowakabili, zikiwemo uhaba wa pembejeo bora na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu mbinu za kisasa za kilimo cha korosho.Kutokana na changamoto hizo, Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa kikao maalum kitaandaliwa hivi karibuni, kitakachowakutanisha wadau wote wa zao hilo ili kujadili suluhisho na kuweka mikakati ya kuimarisha uzalishaji.Alisisitiza umuhimu wa wakulima kubadilika na kuendana na teknolojia ya kilimo cha kisasa ili kuongeza tija na thamani ya zao hilo sokoni. Aidha, alieleza kuwa serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima na wataalamu wa kilimo ili kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji.

“Ni muhimu tukabadilika na kwenda na wakati kwa kutumia mbinu bora za kilimo. Serikali ipo tayari kushirikiana nanyi ili kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chenu,” alisema Mhandisi Mragili.

Aidha, alibainisha kuwa katika kikao hicho, masuala muhimu yatakayojadiliwa ni pamoja na upatikanaji wa pembejeo bora, utoaji wa elimu ya kilimo cha kisasa, na utafutaji wa masoko ya uhakika kwa zao la korosho.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza tija kwa wakulima wa korosho wilayani Bukombe na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Comments