Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadisi Paskasi Mragili, amewataka wazazi na walezi kushirikiana kikamilifu na Serikali kwa kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo ya Polio, ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo hatari usio na tiba.
Wito huo umetolewa leo, Machi 24, 2026, wakati akizindua kampeni maalum ya chanjo ya Polio wilayani humo. Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhadisi Mragili alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Polio yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
“Ugonjwa wa Polio hauna tiba. Tusipochukua hatua madhubuti, tunaweza kupoteza nguvu kazi ya taifa kutokana na athari zake. Ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha mtoto anapata chanjo hii muhimu,” alisisitiza Mragili.
Aidha, aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wote wanashiriki katika kampeni hiyo, hata kama tayari wamekamilisha ratiba ya chanjo za kawaida, ili kuongeza kinga dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Mayunga Mathias, alisema kuwa wilaya imejipanga vyema kuhakikisha inafikia na hata kuvuka lengo la uchanjaji lililowekwa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa zoezi la chanjo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Kalidushi Charles, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika kulinda afya za watoto nchini.
Naye Msimamizi wa zoezi hilo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Stephen Mwaisobwa, alisema mkoa huo utaendelea kushirikiana na halmashauri zote kuhakikisha kila mtoto anayestahili anapatiwa chanjo hiyo bila kukosa.
Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe imelenga kuwafikia na kuwachanja watoto wapatao 156,777 wenye umri chini ya miaka 10 katika kampeni hiyo maalum ya chanjo ya Polio inayoendelea kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026.

Comments
Post a Comment