Wakulima wa zao la korosho wilayani Bukombe mkoani Geita wametakiwa kuzingatia mbinu bora za kilimo kwa kufuata ushauri wa wataalamu na kutumia pembejeo sahihi, ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo muhimu kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadisi Paskasi Muragili, wakati wa kikao maalumu cha wakulima wa korosho kilichofanyika kufuatia ziara yake ya kikazi wiki iliyopita katika Kata ya Namonge, ambako alitembelea mashamba na kusikiliza changamoto zinazowakabili wakulima.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Machi 24, 2026, katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Muragili alisema kikao hicho kililenga kujadili mikakati ya kuboresha uzalishaji, kuongeza ubora wa korosho pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa masoko yenye tija.
Alisisitiza kuwa Serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kilimo bora, pembejeo kwa wakati pamoja na masoko ya uhakika, hatua itakayosaidia kuinua kipato cha wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Naomba mniunge mkono kwa kuwekeza kikamilifu kwenye mashamba yenu kwa kufuata ushauri wa kitaalamu, ili ndani ya miaka mitano uzalishaji wa korosho Bukombe ufikie tani 50,000,” alisema Muragili.
Aidha, aliwataka wakulima kujiunga katika vikundi na vyama vya ushirika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha, mafunzo pamoja na kuwa na nguvu ya pamoja katika masoko. Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto wanazokumbana nazo wakulima mmoja mmoja.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wilayani humo, Zedekiah Osano, alisema juhudi zinaendelea kufanyika za kuwarasimisha wakulima wa korosho ili waweze kutambuliwa rasmi na kunufaika na mpango wa pembejeo za ruzuku.
Osano aliongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe imeanzisha kitalu chenye uwezo wa kuzalisha miche ya korosho 10,000, ambapo hadi sasa miche 6,000 imeoteshwa na kati yake miche 3,000 ipo tayari kwa kupandwa.
Naye mkulima Kalebo Makanu alieleza changamoto zinazowakabili, zikiwemo upatikanaji wa pembejeo bora na athari za mabadiliko ya tabianchi, akiiomba Serikali kuendelea kuwasaidia ili kuongeza uzalishaji.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa makubaliano ya kuanzishwa kwa chama cha ushirika cha wakulima wa korosho, hatua itakayolenga kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha zao hilo linaendelea kuwa chanzo kikuu cha kipato na maendeleo kwa wakulima wa Bukombe.

Comments
Post a Comment